Leo ni siku ya kimataifa ya hewa safi kwa anga la buluu, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guteress ametoa wito kwa mataifa ulimwenguni kufanya kazi kwa pamoja ili kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa kwani uchafuzi wa hewa hautambui mipaka.
Katika ujumbe wake kuhusu siku hii iliyoanzishwa kupitia azimio la mwaka 2019 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Guterres anasema hewa na afya safi ni haki ya binadamu.
Amesema, “Uchafuzi wa hewa unawanyima mabilioni ya watu haki zao. Hewa chafuzi huathiri asilimia 99 ya watu kwenye sayari na watu maskini ambao afya zao huathirika kutokana na joto linalotokana na uhalisia wa maisha yao.
Guterres anafafanua kuwa, “katika maadhimisho haya ya tatu ya Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi kwa Anga ya Buluu, natoa wito kwa nchi zote kufanya kazi pamoja ili kukabiliana na uchafuzi wa hewa.”
Aidha, ameongeza kuwa uwekeza katika nishati mbadala na unahitajika ikiwemo upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, na hatua nyinginezo za kuweza kuokoa mamilioni ya maisha kila mwaka na kupunguza kasi ya mabadiliko ya hali ya tabianchi.
Hata hivyo, ametoa ushauri kwa mataifa duniani kutengeneza sheria ili kukidhi mwongozo wa ubora wa hewa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO na kutoa mipango ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi za magari, mitambo ya kuzalisha umeme, ujenzi, na viwanda.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliteua Septemba 7 kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi kwa anga ya buluu mwaka 2019, na siku ya kwanza iliadhimishwa mwaka wa 2020.
Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi kwa anga ya buluu, inatoa wito kwa kila mtu kuendelea na ushirikiano wa kimataifa, kati ya serikali, mashirika ya kiraia na watu binafsi, kuwahimiza kuchukua hatua kwa ajili ya kupunguza uchafuzi wa hewa na kuleta mabadiliko.