Kikosi cha Azam FC kimewasili salama jijini Dar es salaam kikitokea Mbeya ambako jana Jumanne (Septemba 13) kilicheza mchezo wa Mzunguuko wanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City FC.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, Azam FC ilipata ushindi huo kupitia kwa Mshambuliaji wao kutoka DR Congo Idris Ilunga Mbombo katika dakika ya 61.
Kurasa za Mitandao ya Kijamii za Azam FC zimethibitisha taarifa za kuwasili salama kwa kikosi cha klabu hiyo, huku ikieleza wachezaji wote watapumzika kwa siku mbili kabla ya kurejea kambini kuendelea na maandalizi ya mchezo wa mzunguuko watano wa Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons.
“#ARRIVAL Kikosi chetu kimeshawasili salama jijini Dar es Salaam kwa usafiri wa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kikitokea jijini Mbeya kilipoigagadua Mbeya City jana Jumanne.”
“Wachezaji watapumzika siku mbili kabla ya kurejea mazoezini Ijumaa hii, kuanza maandalizi ya mchezo wetu ujao wa ligi dhidi Tanzania Prisons utakaofanyika jijini Mbeya, Septemba 30.” imeeleza taarifa ya Azam FC
Ushindi wa Azam FC dhidi ya Mbeya City umeifanya klabu hiyo ya Chamazi-Dar es salaam kufikisha alama nane zinazoiweka kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Azam FC imezifunga Kagera Sugar na Mbeya City FC na kutoka sare michezo miwili dhidi ya Geita Gold FC na Young Africans.