Kocha Mkuu wa Geita Gold FC Fred Felix Minziro ameahidi kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Hilal al-Sahil SC ya Sudan.

Geita Gold FC ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa 1-0 Jumapili (Septemba 11), ikiwa ugenini Mjini Omdurman-Sudan hali ambayo imeifanya klabu hiyo ya Geita kuwa na deni la kusaka ushindi wa mabao 2-0 ama zaidi, kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Jumamosi (Septemba 17), Uwanja Azam Complex Chamazi.

Minziro amesema baada ya kikosi chake kuwasili Dar es salaam jana Jumanne (Septemba 13) majira ya Alfajiri, ameanza mikakati ya kukiandaa kikosi chake, ili kufanikisha mpango wa kufanya vyema kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili ambao atakua nyumbani.

Amesema kuna makosa kadhaa ambayo aliyaona kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza na ameanza kuyafanyia kazi kuhakikisha mambo yanawanyookea ili wafuvuzu hatua inayofuata.

“Mchezo wa Kwanza umeshamalizaka kule Sudan, kilichobaki ni kuhakikisha tunashinda mchezo wa Mkondo wa Pili ambao tutakuwa nyumbani, kuna baadhi ya makosa ambayo yalipelekea kupoteza mchezo wetu wa ugenini, hivyo nitatumia muda uliobaki kuwaweka sawa wachezaji wangu.”

“Michezo hii ya hatua ya mtoano imekua na mbinu nyingi hasa unapocheza ugenini ama nyumbani, hivyo ninajua hata wapinzani wetu nao watajipanga kuja kucheza kwa kulinda ushindi wao walioupata, ninaimani wachezaji wangu watatumia kipindi hiki ili kufuata maelekezo nitakayowapa.”

“Ninawaomba watanzani wote bila kujali itikadi zao za kishabiki kuwa pamoja na Geita Gold FC katika mchezo wetu ambao tutacheza hapa nyumbani, mimi kama Kocha nitamaliza kazi yangu katika uwanja wa mazoezi, wachezaji nao watakua na kazi yao Uwanjani lakini Mashabiki tutawahitaji kuja kutupa nguvu ili iwe rahisi kukamilisha lengo la kushinda nyumbani na kusonga mbele.” amesema Minziro

Ikumbukwe kuwa Geita Gold FC ilipata nafasi ya kushiriki katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Tanzania ni sehemu ya nchi zenye nafasi ya uwakilishi wa timu nne katika Michuano ya Kimataifa msimu huu 2022/23, ambapo Upande wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ina timu za Simba SC na Young Africans, huku Azam FC na Geita Gold FC zikishiriki Kombe la Shirikisho.

Geita Gold FC yapewa ushauri wa bure KIMATAIFA
Waombolezaji waonywa ufikiaji mwili wa Malkia