Aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Geita Gold FC na Namungo FC Flugence Novatus amempa ushauri Kocha Fred Felix Minziro kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Hilal al-Sahil SC ya Sudan.
Geita Gold FC ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa 1-0 Jumapili (Septemba 11), ikiwa ugenini Mjini Omdurman-Sudan hali ambayo imeifanya klabu hiyo ya Geita kuwa na deni la kusaka ushindi wa mabao 2-0 ama zaidi, kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Jumamosi (Septemba 17), Uwanja Azam Complex Chamazi.
Novatus amesema bado anaamini Kikosi cha Geita Gold FC kina nafasi kubwa ya kusonga mbele kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Brani Afrika, kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo ambao wanaongozwa na Benchi la Ufundi imara.
Amesema kinachotakiwa kwa sasa ni Kocha Mkuu Fred Felix Minziro kuwaandaa vyema wachezaji wake kimwili na kiakili kuelekea kwenye mpambano huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Soka la Bongo, hasa baada ya kuwa timu pekee ya Tanzania iliyopoteza mchezo wa Kimataifa mwishoni mwa juma lililopita.
“Ninaimani kubwa sana na Kocha Minziro ataweza kufanya kitu katika kipindi hiki cha kujiandaa kuelekea mchezo wa Mkondo wa pili, kikubwa ninamuomba awe mtulivu na abuni mbinu ambazo zitafanikisha lengo linalokusudiwa.”
“Mbali na kuwaandaa wachezaji wake kimwili, pia ninamshauri awaandae kiakili kwa sababu utayari wao ndio utakuwa nyenzo kubwa ya kushinda na kuvuka katika hatua hii ya awali.”
“Geita Gold ina kikosi ambacho kina uwezo wa kufunga zaidi ya bao moja, tumeona katika Ligi Kuu msimu uliopita wamefanya hivyo mara nyingi, kwa hiyo sina shaka nao hata kidogo, kikubwa Benchi la ufundi linapaswa kuwa bega kwa bega katika kipindi hiki ili kufanikisha mikakati ya kuwafurahisha watanzania.” amesema Novatus ambaye aliwahi kuwa Kocha Msaidizi wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Ikumbukwe kuwa Geita Gold FC ilipata nafasi ya kushiriki katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.
Tanzania ni sehemu ya nchi zenye nafasi ya uwakilishi wa timu nne katika Michuano ya Kimataifa msimu huu 2022/23, ambapo Upande wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ina timu za Simba SC na Young Africans, huku Azam FC na Geita Gold FC zikishiriki Kombe la Shirikisho.