Mkuu wa Benchi la Ufundi Dodoma Jiji FC Kocha Masoud Djuma Irambona amesema anaendelea na mikakati ya kuinasua timu yake kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu na kuipeleka katika nafasi za juu.

Dodoma Jiji FC ilianza vibaya msimu huu kwa kufanya vibaya michezo miwili ya awali, kabla ya kulazimisha sare ya bila kufungana dhidi ya Singida Big Stars mwishoni mwa juma lililopita kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida.

Kocha Masoud amesema kwa sasa kikosi chake kinaendelea na maandalizi ya kuelekea mchezo wa mzunguuko wanne, ambapo kitacheza ugenini dhidi ya Kagera Sugar.

Amesema baada ya kuonyesha utayari wa kupambana katika mchezo uliopita dhidi ya Singida Big Stars, amedhamiria kuona kikosi chake kikiendeleza juhudi zaidi kwenye mchezo unaofuata mjini Bukoba mkoani Kagera.

“Tulipambana katika mchezo uliopita na tulidhamiria kupata ushindi lakini bahati haikuwa kwetu wala kwa wapinzani wetu, kilicho mbele yetu kwa sasa ni kuhakikisha tunakwenda Kagera kupata matokeo mazuri ambayo yatatuondoa katika nafasi za mwisho kwenye msimamo wa Ligi.”

“Dhamira yangu na wenzangu katika Benchi la Ufundi ni kuona timu yetu inafanya vizuri, tayari tumeonyesha mwanga baada ya kupambana vizuri tulipocheza mjini Singida mwishoni mwa juma lililopita, nina uhakika Mungu atatusaidia tutafanya vizuri kwenye mchezo wetu na Kagera Sugar.”

“Tumejipanga kuhakikisha tunapata alama kadhaa katika michezo iliyo mbele yetu, hii ni siri yetu sisi makocha, wachezaji na viongozi wa timu, tukifikia lengo tunaamini tutakuwa katika mahala salama na Dododma Jiji itamfurahisha kila shabiki wake.” amesema Kocha Masoud Djuma

Dodoma Jiji FC itakua ugenini Jumapili (Septemba 18), ikicheza dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.

RASMI Mo Simba Arena kuzunguushiwa ukuta
Geita Gold FC yapewa ushauri wa bure KIMATAIFA