Mwakilishi wa Mkandarasi Kampuni ya Mega Woodcraft, Jonathan Kibona ametoa sababu za Kampuni yao kushindwa kuanza ujenzi wa Ukuta katika Uwanja wa Mo Simba Arena kwa wakati uliokua umekusudiwa.
Simba SC imekua ikiutumia Uwanja wa Mo Simba Arena kwa vikosi vyake vyote, kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kuajiandaa na Michauno mbaliambali, lakini eneo hilo limekua na changamoto ya kukosa ukuta kwa muda mrefu.
Kibona amezungumza na Waandishi wa Habari waliofika Uwanjani hapo leo Jumatano (Septemba 14), kufuatia ziara iliyofanywa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla kwa ajili ya kukagua mipaka ya Uwanja wa Mo Simba Arena.
Kibona mesema zoezi la kuzunguushia ukuta katika Uwanja wa Mo Simba Arena lilishindwa kuanza kwa wakati kutokana na uvamizi wa baadhi ya maeneo katika uwanja huo.
“Zoezi lilichelewa sababu kulikuwa na uvamizi lakini baada ya maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na vifaa vipo tayari ndani ya miezi miwili na nusu uzio madhubuti utakuwa tayari.” amesema Kibona
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ‘RC’ Amos Makalla amemaliza mgogoro wa Ardhi katika kiwanja namba 229 Kinachomilikiwa na Simba SC maeneo ya Bunju B Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
RC Makalla baada ya kuzuru eneo la kiwanja alipata wasaa wa kujionea mipaka na Wananchi takribani 9 ambao wamevamia na kujenga katika eneo hilo.
Aidha RC Makalla amewataka wananchi waliovamia katika kiwanja hicho ndani ya siku 60 kuanzia leo Jumatano (Septemba 14) kujipanga kuondoka mara moja kwa kuwa eneo hilo ni mali halali ya Simba SC ndio wenye hati miliki.