Baada ya kuibuka kwa taarifa ya kufungiwa kwa Muda usiojulikana kupanda ulingoni katika Ardhi ya Uingereza, Bondia Hassan Mwakinyo ameibuka na kuwataka Watanzania kuacha Mihemko.
Jana Jumatatu (Septemba 19), Vyanzo mbalimbali vya habari nchini Tanzania viliripoti taarifa za kufungiwa kwa Bondia huyo kutoka jijini Tanga, hali ambayo ilizua taharuki kubwa.
Hata hivyo taarifa hizo hazikueleza sababu za Mwakinyo kufungiwa kucheza masumbwi ya kulipwa nchini Uingereza.
Mwakinyo ametumia ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Twitter kutoa ufafanuzi wa adhabu hiyo kwa kueleza kwa kina sababu ambazo zimeifanya Bodi ya Ngumi za Kulipwa Nchini Uingereza (BBBC) kutangaza kumfungia kucheza ngumi nchini humo.
Mwakinyo ameandika: “Bondia anapopoteza pambano kwa TKO au KO kwa sheria za Uingereza anatakiwa kupumzika kwa siku 45, kutokana na hali hiyo haimaanishi kuwa nimefungiwa, hivyo punguzeni mihemko.”
Ikumbukwe kuwa Hassan Mwakinyo alipoteza pambano lake dhidi ya Bondia wa Uingereza Liam Smith kwa TKO Septemba 03, na tayari taarifa zinaeleza kuwa wawili hao watazichapa tena mapema mwezi Januari 2023.