Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kufanya tafiti za madini katika Wilayani Kilombero, Morogoro na Wilaya ya Mufindi ya Njombe ili kubaini aina ya madini yaliyopo maeneo hayo.
Dkt. Kiruswa ametoa agizo hilo, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Abubakari Asenga wakati wa kipindi cha maswali na majibu kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma hii leo Septemba 20, 2022.
Amesema, Taasisi ya GST imefanya utafiti wa awali sambamba na kuchora ramani kwenye maeneo yote yaliyopo katika Jimbo la Kilombero katika mfumo wa Quarter Degree Sheet (QDS).
Dkt. Kiruswa, ameainisha maeneo mbalimbali yenye madini ya dhahabu na vito yaliyopo Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro, ambapo tafiti za awali zilizofanyika katika Wilaya humo zilionesha uwepo wa madini hayo katika Kata ya Chisano.
Aidha ameongeza kuwa, GST ilifanya utafiti wa awali na kuchora ramani ya eneo la Hifadhi ya Milima Udzungwa na maeneo jirani ambapo utafiti wa madini uliofanyika katika maeneo hayo hauoneshi taarifa zozote za uwepo wa madini ya thamani katika milima hiyo.
Mkoa wa Morogoro, umebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za madini ikiwemo dhahabu, Shaba, Kinywe, madini ya viwandani (Ulanga, Kaoline), madini ya ujenzi (mchanga, kifusi) na madini ya vito ( Rubi, Rodolite).