Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeisisitiza Wizara ya Maji na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), kumaliza kabla au kwa wakati mradi wa maji unaotekelezwa katika Kata ya Nzuguni iliyoyopo jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Christine Ishengoma ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo wa maji unaotarajiwa kuhudumia wananchi 33,000 wa Mitaa ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa.
Amesema, “Nawaomba mmalize mradi huu ndani ya miezi sita mliyoahidi au kabla ya miezi hiyo ili wananchi wasiendelee kuteseka na kero hii eneo hili la Nzuguni wananchi wake walikuwa na changamoto kubwa ya maji, tatizo hili linaenda kutatuliwa kupitia visima hivi vitano vilivyochimbwa vinavyotoa maji safi na salama yasiyo na chumvi.”
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuwa wizara hiyo iliwaelekeza Wataalam wake kuyatafuta maji popote yalipo ili kuhakikisha Kata ya Nzuguni inaondokana na ukosefu wa huduma za maji safi, salama na yenye kutosheleza.
Amesema, “Wataalam wetu wamefanya kazi nzuri ambayo inatupa matumaini kuwa tatizo la maji katika Kata hii linakaribia kutatuliwa kwani mahitaji ya maeneo haya ni jumla ya lita milioni 4 na mradi huu unatarajiwa kuzalisha lita milioni 6, hivyo tutakuwa na maji yanayotosheleza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema mradi huo wa maji Nzuguni umegharimu Shilingi bilioni 4. 56 na utaongeza uzalishaji wa maji jijini Dodoma, kutoka lita milioni 67.8 hadi lita milioni 73.8 kwa siku, sawa na ongezeko la asilimia 9.