Kocha Mkuu wa Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’ Patrick Odhiambo amesema kikosi chake kipo tayari kwa mpambano wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC.
Tanzania Prisons itakua mwenyeji wa Azam FC katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya keshokutwa Ijumaa (Septemba 30).
Kocha huyo kutoka nchini Kenya amesema kwa siku kadhaa kikosi chake kimekua kikifanya maandalizi ya kuelekea mchezo huo, huku kila mchezaji akionyesha kuwa tayari kuingia katika vita ya kuziwania alama tatu muhimu.
Odhiambo amesema lengo kuu la kuelekea katika mchezo huo ni kuhakikisha wanashinda, ili kurejea katika njia ya ushindi, baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Simba SC uliopigwa mwanzoni mwa mwezi huu jijini Mbeya.
Amesema wanaiheshimu Azam FC kutokana na kuwa na kikosi bora na imara, na msimu huu wameanza vizuri, kwani hadi sasa hawajapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu.
“Katika kipindi hiki cha mapumziko ya kupisha michezo ya Kalenda ya FIFA imetusaidia sana kujiandaa kuelekea mchezo wetu dhidi ya Azam FC, lengo letu ni kuhakikisha tunashinda mchezo huo ili kuwa katika njia salama ya kurejesha furaha kwa mashabiki wetu,”
“Kama unavyojua mchezo uliopita tuliocheza hapa Mbeya dhidi ya Simba SC tulipoteza, hivyo mchezo dhidi ya Azam FC tena nyumbani tunalazimika kupambana kwa hali yote ili tupate matokeo mazuri.”
“Tunaipa heshima zote Azam FC kwa sababu msimu huu ipo katika sura nzuri ya kiushindani, imetoka kushinda hapa dhidi ya wenzetu wa Mbeya City, hivyo imetulazimu kujiandaa kwa msingi hiyo ya kuchukua tahadhari ili kufanikisha lengo la kutopoteza mchezo wapili mfululizo hapa.” amesema Kocha Odhiambo
Azam FC itacheza ugenini keshokutwa Ijumaa (Septemba 30), huku ikiwa na rekodi nzuri msimu huu baada ya kushika dimbani mara nne na kuambulia ushindi mara mbili na sare mbili, zinazoifanya timu hiyo ya Chamazi kufikisha alama 08 zinazoiweka kwenye nafasi ya nne kwenye msimamo.
Tanzania Prisons nayo imeshashuka dimbani mara nne msimu huu, ikishinda mchezo mmoja, kutoka sare mara moja na kupoteza mara mbili, hali inayoifanya klabu hiyo kufikisha alama 04, zinazoiweka kwenye nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu.