Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema safari ya kuelekea Angola itakua na malengo makuu mawili katika michuano ya Kimataifa Barani Afrika upande wa klabu hiyo ya Msimbazi.
Simba SC itacheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Angola Premeiro De Agosto, Jumapili (Oktoba 09) Estádio França Ndalu mjini Luanda-Angola, kisha mchezo wa Mkondo wa Pili utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Jumapili (Oktoba 16).
Ahmed Ally amesema lengo la kwanza kuelekea mchezo huo ni kuhakikisha kikosi chao kinapambana na kupata ushindi dhidi ya wenyeji wao, huku lengo la pili likiwa ni kufuta rekodi mbaya kila wanapocheza nchini Angola.
“Tutaondoka Jumamosi October 08/2022 kwenda Angola ambapo tutacheza Mchezo wetu October 9/2022. Tunaenda Angola sio tu kucheza bali kufuta historia mbaya iliyowahi kutokea hapo awali”
“Mara ya mwisho Simba kwenda Angola kwenye michuano ya (CAF) tulipoteza (5-0) dhidi ya Libolo FC. Tunakwenda kuifuta hiyo historia licha ya kwamba tunacheza na timu tofauti na Libolo FC ” amesema Ahmed Ally
Simba SC ilitinga hatua ya kwanza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kufuatia ushindi wa jumla wa 4-0 dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Malawi Nyasa Big Bullet, huku Premeiro De Agosto inayomikiwa na Jeshi la Angola, ikipata nafasi hiyo kwa kuitoa Red Arrows ya Zambia kwa ushindi wa jumla wa 2-1.