Serikali nchini Ethiopia, imekubali mito wa Umoja wa Afrika (AU), kushiriki kwenye mazungumzo ya kutafuta amani ya mzozo wa Tigray bila ya kutoa masharti yeyote hatua mbayo imepongezwa na baaadhi ya Mataifa.
Mshauri wa Waziri Mkuu kuhusu usalama wa Kitaifa, Redwan Hussein amethibitisha hayo hii leo Oktoba 5, 2022 na kusema hatua hiyo ni mwangaza wa utafutaji wa amani ya eneo hilo na nchi jirani.
Mazungumzo hayo, yatanatarajia kufanyika nchini Afrika Kusini mwishoni wa wiki hii, yakilenga kumaliza machafuko ambayo yamedumu kwa miaka miwili sasa.
Hata hivyo, vikosi vya Tigray bado havijatoa jibu kama vitashiriki mazungumzo hayo, lakini kulingana na duru mbili za kidiplomasia huenda huo ukawa ni mwanzo wa mazungumzo rasmi ya kwanza kati ya pande hizo mbili tangu vita vilipoanza Novemba 2020.
Awali, pande zote mbili zilisema ziko tayari kwa mazungumzo ya amani chini ya Umoja wa Afrika, lakini mapigano makali yamekuwa yakiendelea jimbo la Tigray na kusababisha vifo na mamilioni ya watu kulazimika kuyakimbia makazi yao.
Wito wa kutafuta amani ya Tigray, umekuwa ukitolewa na Mataifa mengi Ulimwenguni, ili kunusuru maisha ya watu wasio na hatia ambao wameathiriwa na vita hiyo.