Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari kwa ulimwengu juu ya matumizi ya dawa nne za kikohozi ambazo zimetajwa kuwa zinaweza kuhusishwa na vifo vya watoto 66 nchini Gambia.
Bidhaa hizo zinazotengenezwa na kampuni ya Kihindi, Maiden Pharmaceuticals, lakini “zina uwezekano wa kuhusishwa na majeraha ya figo na vifo 66 kati ya watoto,” taarifa hiyo ilisema na kuzitaja dawa hizo kuwa ni Promethazine Oral Solution, Kofexmalin Baby Cough Syrup, Makoff Baby Cough Syrup na Magrip N Cold Syrup.
Taarifa hiyo ya WHO inaongeza kuwa bidhaa hizo nne zilitambuliwa nchini Gambia, lakini huenda zilisambazwa, kupitia masoko yasiyo rasmi, kwa nchi au kanda nyingine.
WHO imetoa taarifa hiyo baada ya mamlaka ya matibabu nchini Gambia kugundua ongezeko la matukio ya majeraha ya papo hapo ya figo miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano mwishoni mwa mwezi Julai.
‘Panya road’ 40 wafikishwa Mahakamani
Hata hivyo serikali ya Gambia tangu Julai imesitisha matumizi ya dawa zote za maji zenie mchanganyiko wa paracetamol na imewataka watu kutumia vidonge badala yake.
WHO ilisema kwamba uchambuzi wa kimaabara wa sampuli za bidhaa unathibitisha kuwa zina kiasi kisichokubalika cha ‘diethylene glikoli’ na ‘ethilini glikoli’ kama vichafuzi vyenye sumu, na athari zake zinaweza kujumuisha maumivu ya tumbo, kutapika, kuhara, kushindwa kutoa mkojo, maumivu ya kichwa, hali ya kiakili iliyobadilika na jeraha la papo hapo la figo ambalo linaweza kusababisha kifo iliongeza.
Katika taarifa yake Katibu mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus alisema kupoteza maisha ya vijana wengi ni jambo la kuvunja moyo kwa mataifa na kwa familia zao.
Nchi zote ambazo zimefikiwa na dawa hizo zimeshauriwa kutosambaza kwa wananchi wake kwani inawezekana ziliwafikia kwa njia ambazo sio za halali.