Kufuatia Jeshi la Polisi nchini, kuwataka wahitimu wa darasa la saba waliomaliza mitihani yao Oktoba 6, 2022 kote nchini kudumisha nidhamu na utii baadhi ya Wazazi na Walezi wamesema suala hilo litawezekana iwapo ushirikiano baina ya jamii utapewa kipaumbele.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti hii leo Oktoba 7, 2022, baadhi ya wazazi na walezi wamesema uporomokaji wa maadili umekuwa ukichangiwa na sababu nyingi ikiwemo hali ya usasa na kutokuheshimu mila na desturi za Taifa au kabila za ukoo mbalimbali nchini.
Mmoja wa walezi hao, Daniel Mgube (47), amesema, “Maadili yameporomoka, na Polisi inatakiwa kutambua kuwahimiza watoto pekee haitoshi bali inatakiwa kuhimiza jamii nzima kulichukulia jambo hili kwa mapana na kwa uzito kwani watoto hawa wanazungukwa na mambo mengi sana sote ni mashahidi,”
Naye, mzazi wa mtoto aliyemaliza darasa la saba, Hellen Pius (37), amesema, “Tutawaonea bure hawa maana kuharibika kwao kunatokana na sisi, tubadilike kwanza sisi na wao wataiga, kuna kauli au maagizo mengine huwa yanatafakarisha sana lakini tunanyamaza tu maana waweza ongea ukaeleweka tofauti.”
Mapema hapo jana (Oktoba 6, 2022), Jeshi la Polisi liliwataka wahitimu wa darasa la saba kujitunza, kutojihusisha katika vitendo vya kihalifu kama vile uvutaji bangi, ulevi, uasherati, kuangalia picha za ngono pamoja na kuepuka kujiingiza katika vikundi vya kihalifu.
Kupitia kwa Msemaji wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, David Misime wakati akizungumza na Wahitimu wa darasa la saba katika shule ya msingi Mlezi iliyopo jijini Dodoma, alisisitiza juu ya umuhimu huo wa kutokushiriki vitendo visivyofaa.