Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Sudan Al Hilal Florent Ibenge, amesema wamekuja Tanzania kupambana na kusaka matokeo yatakayowawezesha kutinga hatua ya Makundi, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Al Hilal kesho Jumamosi (Oktoba 08) itakua mgeni wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa kumi jioni.

Kocha Ibenge ambaye hakuwahi kucheza na Young Africans kwenye Michuano ya Kimataifa zaidi ya kukutana na Simba SC kwa nyakati tofauti akiwa na AS Vita ya DR Congo na RS Berkane ya Morocco, amesema anawafahamu vizuri wapinzani wake, na amekiandaa kikosi chake kutokana na kufahamu anachokifahamu.

Amesema Wachezaji wengine wanaounda kikosi cha Young Africans kwa sasa, wana uzoefu mkubwa wa kupambana Kimataifa na hatua hiyo ndio iliyomuengezea chachu ya kufanya maandalizi makubwa ya kikosi chake kilichowasili Dar es salaam jana Alhamis (Oktoba 06), kikitokea DR Congo kilipokua kimeweka Kambi ya siku Sita.

“Najua Young Africans ina wachezaji wakubwa wenye uzoefu wa michuano hii, lakini naiamini timu yangu nawaamini vijana wangu wataonyesha mchezo mzuri, kwa sababu ninazo mbinu ya kufuzu hauta ya Makundi”

“Young Africans imekua na muendelezo mzuri wa kupata matokeo ya ushindi katika Ligi ya Tanzania, ninafuatilia kila hatua yao, lakini hii ni michuano ya Afrika, na ndio maana tunapambana mabingwa wa nchi za Afrika.”

“Naamini wao wamejiandaa kutukabili sisi, na sisi tumejiandaa kuwakabili wao, kwa hili ninaamini tutakuwa na mchezo mzuri sana kesho hapa Dar es salaam, tutashuhudia soka safi kwa sababu tupo hapa kupambana na kusaka ushindi.” amesema Frolent Ibenge

Young Africans ilitinga Mzunguuko wa Kwanza kwa matokeo ya jumla 9-0 dhidi ya Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC, huku Al Hilal ikisonga mbele kwa faida ya bao la ugenini, kufutia ushindi wa jumla wa sare ya 2-2.

Ikicheza ugenini Ethiopia dhidi ya St George mwezi Septemba Al Hilal ilikubali kufungwa 2-1, kabla ya kuibuka na ushindi wa 1-0 mjini Khartom.

Panya auwa watu 37, wamo watoto 24
Vita Ukraine: Putin akabiliwa na upinzani wa ndani