Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema haikuwa rahisi kupata ushindi ugenini kama inavyochukuliwa na baadhi ya Mashabiki wa klabu hiyo, ambao leo Jumatatu (Oktoba 10) wameamka na furaha.

Simba SC jana Jumapili (Oktoba 09) ilicheza ugenini Luanda-Angola dhidi ya Mabingwa wa nchi hiyo Primeiro De Agosto katika mchezo Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kupata ushindi wa 3-1, ambao unawaweka katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya Makundi.

Kocha Mgunda amesema ilikua vigumu sana kucheza katika Uwanja wa ugenini, lakini usikivu na umakini wa wachezaji wake ulifanikisha lengo lililowapeleka Angola na mwishowe kuibuka kidedea.

Amesema jambo la kwanza alilowahimiza wachezaji wake ni kuwa na nidhamu dhidi ya wenyeji wao, ambao walikua wana kila sababu ya kuutumia vizuri Uwanja wao wa nyumbani, lakini walifanikiwa kuwadhibiti na kuwashangazwa kwa ushindi waliouvuna ugenini.

“Primeiro De Agosto sio wa kawaida kama inavyochukuliwa na baadhi ya Mashabiki, hawa ni Mabingwa wa Angola, kwa hiyo tumecheza na Mabingwa katika Ligi yao”

“Kikubwa niliwataka wachezji wangu kuwaheshimu kwa nafasi yao ya kuwa Mabingwa, pia niliwataka kupambana kwa kuwapa nafasi ya wao kucheza katika eneo lao bila kutupa madhara kwenye eneo letu, nashukuru kwa hilo tulifanikiwa.”

“Michezo hii ina mbinu nyingi sana, tulichokifanya sisi ni kutumia nafasi tulizozipata kutokana na makosa ya wenzetu, wachezaji wangu walikua makini na wakakamilisha kazi iliyotupeleka Angola.” amesema Kocha Mgunda

Kuhusu mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumapili (Oktoba 16) kocha huyo mzawa wamesema bado kazi ni kubwa kwa kikosi chake kuhakikisha kinapambana na kufanikisha mpango wa kutinga hatua ya makundi.

“Lazima tutambue kwamba mchezo wa mpira unapofunga nawe lazima utafungwa, kwa hiyo kama tumewafunga kwao inawezekana na wao wakaja kutufunga hapa, huu mchezo haujamalizika ni kama tumemaliza kipindi cha kwanza sasa tunakwenda kipindi cha pili lolote linaweza kutokea.”

“Nitakachokifanya ni kuwaandaa wachezaji wangu kuelekea mchezo huo, lengo letu ni kupambana na kuendeleza mazuri tuliyoyapata ugenini, na wao watakuja wakiwa na lengo la kurekebisha makosa yao.” amesema Mgunda

Tayari kikosi cha Simba SC kimeshawasili jijini Dar es salaam majira ya Alfajiri kikitokea Luanda-Angola kilipokuwa na kazi kubwa ya kuikabili Primeiro De Agosto.

Mimi ndiye mhalifu mkuu, niadhibiwe: Museveni
Try Again ahimiza umoja, mshikamano Simba SC