Kiungo wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Feisal Salum ‘Fei Toto’ ametangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Septemba wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwashinda Washambuliaji Mosses Phiri (Simba SC) na Reliants Lusajo (Namungo FC).

Fei Toto ametajwa kuwa mshindi wa Tuzo hiyo, kufuatia maamuzi ya Kikao Kamati ya Tuzo ya TFF kilichokutana mwishoni mwa juma lililopita jijini Dar es salaam.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu ‘TPLB’ imeeleza kuwa Kiungo huyo wa Young Africans, amewashinda wapinzani wake baada ya kuonesha kiwango kizuri kwa mwezi Septemba na kutoa mchango mkubwa kwa klabu yake, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili.

Katika hatua nyingine taarifa hiyo imemtaja Kocha Honour Janza wa Namungo FC kama Kocha Bora wa mwezi Septemba akiwashinda Charles Mkwasa (Ruvu Shooting) na Thiery Hitimana (KMC FC).

Kwa mwezi Septemba Kocha Janza alikiongoza kikosi cha Namungo FC kushinda dhidi ya Ruvu Shooting 1-0 na kisha Coastal Union 1-0.

Wakati huo huo Kamati ya Tuzo za TFF imemtangaza Elisha Kimanzi kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa Mwezi Septemba.

Kimanzi ni Meneja wa Uwanja wa Majaliwa, uliopo mkoani Lindi ambapo unatumiwa na klabu ya Namungo FC katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Rwanda yajipigia chapuo wakimbizi nchi za Magharibi
Urusi yatangaza Jenerali mpya wa vita