Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amesema hana mashaka na mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Hilal utakaopigwa Omdurman-Sudan.
Young Africans itacheza ugenini Jumamosi (Oktoba 15), baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Jumamosi (Oktoba 08), hali ambayo iliibua taharuki kwa baadhi ya Mashabiki ambao waliamini huenda mambo yangewaendelea vizuri nyumbani.
Kocha Nabi amesema ameanza mikakati wa kukiandaa kikosi chake kuelekea mchezo huo, huku akiwa na matumaini makubwa ya kupata matokeo mazuri ugenini.
Amesema ana wachezaji wazuri ambao wana uwezo wa kupambana katika Uwanja wa nyumbani na Viwanja vya ugenini, hivyo hana mashaka yoyote kuelekea mchezo dhidi ya Al Hial.
“Bado tunayo nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo wetu wa marejeano, Young Africans tuna wachezaji wazuri ambao wana uwezo wa kupambana popote, iwe nyumbani ama ugenini,”
“Kwa upande mwingine tumeshawaona wapinzani wetu jinsi wanavyocheza, hivyo katika mchezo wetu wa ugenini tutaweka mipango mizuri ya kupambana na kuhakikisha tunashinda.” Amesema Nabi
Katika mchezo huo Young Africans italazimika kusaka ushindi wa aina yoyote ama matokeo ya sare kuanzia 2-2 na kuendelea, ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Maingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Mara ya mwisho Young Africans kutinga hatua ya Makundi kwenye michuano hiyo ilikua mwaka 1998.