Serikali ya nchi ya Gambia, imepanga kuimarisha hatua za kiafya ikiwa ikiwa ni pamoja na udhibiti bora wa ubora wa dawa zinazoagizwa kutoka nje, baada ya vifo vya kushangaza vya watoto 66.
Rais wa Gambia, Adama Barrow ameyasema hayo wakati akihutubia Taifa hilo na kusema, “Ndugu zangu wananchi wa Gambia, wakazi wa Gambia, ninawahakikishia wote kwamba Serikali haitaacha lolote ili kupata undani wa tukio hili.”
Aidha ameongeza kuwa, “Wizara ya Afya inachunguza chanzo cha dawa zilizochafuliwa, mazingira na taratibu za uingizaji wa dawa nchini na kuweka ulinzi ili kutokomeza uingizaji wa dawa zisizo na viwango.”
Gambia, ilizindua kampeni ya dharura ya nyumba kwa nyumba kuondoa dawa za kikohozi na baridi zinazolaumiwa kwa vifo vya watoto 66 vilivyosababishwa na figo zao kushindwa kufanya kazi katika muda wa miezi mitatu iliyopita.
Rais Barrow amesema, mlipuko huo sasa umedhibitiwa, na kwasasa ni kesi mbili pekee ambazo zimeripotiwa katika wiki mbili zilizopita hali inayoonesha matumaini na kufanya Serikali yake kuweka juhudu zaidi ili kudhibiti tatizo hilo.
Oktoba 5, 2022, Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, lilitoa tahadhari juu ya dawa nne za kikohozi na baridi zilizotengenezwa na Maiden Pharmaceuticals ya nchini India, kuwa huenda zilichangia vifo na kwamba linafuatilia uchunguzi na kampuni hiyo kwa kushirikiana na mamlaka za udhibiti nchini India.