Kikosi cha KMC FC kesho Jumamosi (Oktoba 15) kitaendelea na Mshike Mshike wa kusaka alama tatu muhimu za Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kuikabili Mtibwa Sugar iliyofunga safari kutoka Manungu Mkoani Morogoro.
Mchezo huo umepangwa kupigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam kuanzia saa kumi jioni, huku kila upande ukikumbuka matokeo ya sare waliopatikana katika michezo yao iliyopita.
Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni, inayonolewa na Kocha Mkuu Thierry Hitimana imefanya maandalizi ya mwisho na imejinasibu kuwa tayari kwa mtanange huo, ambao unatabiriwa kuwa na ushindani mkubwa.
Afisa Habari na Mawasiliano wa KMC Christina Mwagala amesema pamoja na ushindani uliopo katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kikosi chao kimejiandaa kinapata ushindi muhimu dhidi ya Mtibwa Sugar.
“Tunakwenda kwenye mchezo mwingine tukiwa nyumbani, tunawaheshimu wapinzani wetu Mtibwa Sugar kwa kuwa ni Timu nzuri na wao pia wanahitaji matokeo, lakini pamoja na hayo kama Manispaa ya Kinondoni tumejipanga kupata ushindi licha ya kwamba katika mchezo uliopita tulipata sare hapa nyumbani.”
“Tuna amini kuwa matokeo mazuri tutayapata kutokana na kwamba KMC FC tunawachezaji wazuri na wenye ubora mkubwa ambao wanaweza kupambana kutafuta matokeo, na siku zote Timu Bora huwa haitoki sare mara mbili kwenye uwanja wa nyumbani.”
Katika hatua nyingine Afisa Habari na Mawasiliano wa KMC Christina Mwagala amesema wachezaji wote wako vizuri isipokuwa Ibrahimu Ame, Emmanuel Mvuyekure pamoja na Kelvin Kijili ambao wanakabiliwa na changamoto ya majeraha walioyapata wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya Mbuni FC uliochezwa Jumanne (Oktoba 11) na kuambulia sare ya bila kufungana.