Droo ya Hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika itafanyika leo Jumanne (Oktoba 18) mjini Cairo-Misri, huku Young Africans ya Tanzania ikisubiri mpinzani wake ambaye atacheza naye michezo miwili ya kuamua kwenda Hatua ya Makundi.
Young Africans iliingia kwenye Mchato huo, kufuatia kuondolewa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa na Mabingwa wa Sudan Al Hilal 1-0 juzi Jumapili (Oktoba 16) mjini Khartoum.
Habari njema kwa Young Africans katika Droo hiyo ni kwamba, haiwezi kukutana na klabu ambazo zimeondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kama TP Mazembe ( DR Congo), Al Ahli Tripoli (Libya ), ASEC Mimosas (Ivory Coast ), 1º de Agosto (Angola ), Royal Leopards (Eswatini), Flambeau du Centre (Burundi ), Djoliba (Mali), ASN Nigelec (Niger).
Nyingine ni Plateau United (Nigeria), Rivers United (Nigeria), La Passe (Shelisheli), Cape Town City (Afrika Kusini), ASKO Kara (Togo) na US Monastir (Tunisia).
Mpinzani wa Young Africans atatoa kwenye kundi la Klabu ambazo zilishiriki Kombe la Shirikisho msimu huu na kufuzu hatua inayofuata kama Ashant (Guinea), Al Akhdar (Libya), Diables (Congo Brazzavile), DC Motema Pembe (DR Congo), Club Africain (Tunisia), Future FC (Misri) na Malumo Gallant (Afrika Kusini).
Nyingine ni Royal AM (Afrika Kusini), Saint Lupopo (DR Congo), Pyramids (Misri), Real Bamako (Mali), USM Algers (Algeria), CS Sfaxien (Tunisia) na MAbingwa watetezi RS Berkane (Morocco).
Michezo ya Mkondo wa Kwanza Hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika imepangwa kuchezwa kati ya Novemba 02, huku Michezo ya Mkondo wa Pili ikipangwa kupigwa Novemba 09.