Serikali nchini Tanzania, imesema ipo tayari kupeleka Miundombinu ya Mawasiliano katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kupitia Ziwa Tanganyika.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa Kongamano la Fursa za Kibiashara na Uwekezaji katika Sekta ya TEHAMA lililoanza leo jijini Lubumbashi, DRC.

Amesema, “Serikali ya Tanzania iko tayari kuleta miundombinu ya mawasiliano ya Tanzania hususani Mkongo wa Taifa ili kuiunganisha DRC na nchi jirani na tunaamini katika umoja na ushirikiano wa nchi zetu kushirikiana ili kufikia malengo ya kiuchumi ya nchi zetu.”

Awali, Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Said Mshana amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji wa TEHAMA wa DRC kuwa, Tanzania ni nchi iliyojipanga kufanya biashara na DRC.

Amesema, “Tanzania na DRC ni soko la zaidi ya watu 160 na hivyo ushirikiano baini yetu ni muhimu, tukishirikiana pamoja tutakuwa na nafasi nzuri sana ya kuleta maendeleo kwa nchi zetu.”

Kongamano hilo, linafanyika ikiwa miezi miwili tu tangu Viongozi wa nchi hizo mbili wakutane nchini DRC, wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu 'aikataa' Hospitali ya Namtumbo
Zelensky alia na Urusi mauaji ya raia