Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameonesha kutoridhishwa na miundombinu ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo iliyopo Mkoani Ruvuma, na kusema Serikali haitanyamaza kuona baadhi ya watumishi wakifanya vitendo vya hovyo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo hilo leo Oktoba 18, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Migelegele mara baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.

Amesema, “Nimekagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya lakini sijaridhishwa na nimeagiza milango yenye hitilafu yote ing’olewe iwekwe yenye hadhi, iweje imeacha nafasi juu hadi vidole vinapita? mtu akifunga mlango wewe uliyeko nje unaona ndani hii haikubaliki.”

Akikagua ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Mkuu alikuta baadhi ya milango imepishana urefu licha ya kuwa inapaswa ikutane ili kitasa kiweze kufunga na mingine kugoma kufunga, kurudi nyuma na kubakia wazi.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo kushughulikia mapungufu yaliyojitokeza ili kuweza kuipahadhi Hospitali hiyo.

Walimu waadhibiwa kwa utoro kazini
Serikali kupelekea miundombinu ya mawasiliano DRC