Mchambuzi wa Michezo nchini Tanzania Jemedari Saidi Kazumari amesema umefika wakati kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kuthibitisha ubora wao Kimataifa, kupitia Michuano ya Kombe la Shirikisho.

Young Africans ilitupwa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa mwishoni mwa juma lililopita kwa kufungwa na Al Hilal ya Sudan kwa ushindi wa jumla wa 2-1.

Jemedari amesema kitendo cha Klabu hiyo ya Dar es salaam kupangwa na Club Africain kinatakiwa kupokela kama sehemu ya kudhihirisha ubora na ukubwa wake katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema Young Africans imekua na mwenendo mzuri tangu msimu uliopita na imepata mafanikio kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na tuzo kadhaa kupitia kwa wachezaji na Kocha Mkuu Nasredeen Nabi, hivyo kupangwa na Club Africain ya Tunisia inatakiwa kuonyesha kitu ndani ya dakika 90 za nyumbani na ugenini.

“Club Africain ni aina ya timu ambayo Yanga SC inapaswa kuthibitisha ubora wake, mabingwa wa Ligi Kuu Bara bila kufungwa na mechi 42 za Ligi Kuu bila kupoteza, ubingwa wa FA Cup, kocha bora wa msimu, kipa bora, kiungo bora, beki bora, mchezaji bora wa msimu, wapi tena kama sio hapa” amesema Jemedari

Katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho hatua ya mtoano, Young Africans itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Novemba 02, kisha itakwenda Tunisia kwa mchezo wa Mkondo wa pili uliopangwa kuchezwa Novemba 09 jijini Tunis.

Mshindi wa jumla katika mchezo huo ataungana na klabu nyingine 15 zitakazotinga hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho msimu huu 2022/23.

Kocha Juma Mgunda aipa jeuri Simba SC
KMC FC kuikaribisha Azam FC Uwanja wa Uhuru