Meneja wa Habari na Mawasilino wa Klabu ya Simba SC Ahmed Ally ametamba kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans, huku akiwataja baadhi ya wachezaji wanaounda kikosi cha Mnyama.

Wachezaji Moses Phiri, Clatous Chotta Chama na John Bocco ni sehemu ya wachezjai waliotajwa na Ahmed Ally, akiamini watatosha kuimaliza Young Africans Jumapili (Oktoba 23), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Ahmed Ally amesema Simba SC inaendelea kujiamini kama ilivyofanya katika michezo iliyopita ikiwemo ya Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa, hivyo hawatishwi na lolote kuelekea mchezo wa Jumapili (Oktoba 23).

Amesema kikosi chao kipo imara na kwa sasa kinaandaliwa vizuri na Kocha Juma Mgunda, ambaye amedai anafahamu vizuri namna ya kuibali Young Africans katika michezo namna hiyo.

“Kwenye Michezo yetu yote ambayo tunacheza tunapata nguvu ya kujiamini kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa ikiwa ni pamoja na Phiri, Chama, Bocco, Jonas Mkude na wengine wengi, hawa hawatumii muda mwingi kufundishwa, wanajielewa na wanafanya kazi.”

“Tunafahamu mchezo dhidi ya Young Africans utakuwa mgumu, kuna balaa zito linakwenda kufanyika na kila mchezaji anajuwa nini malengo yetu msimu huu, hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi kuona burudani ya kweli.” amesema Ahmed Ally.

Phiri anaongoza kwa wachezaji wenye mabao mengi Simba SC katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, akiwa ameshafunga mabao manne.

Abdul Sopu kuikosa KMC FC kesho
Wawili kuondoka Young Africans Dirisha Dogo