Mshambuliaji Abdul Seleman Sopu ataukosa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC utakaopigwa kesho Ijumaa (Oktoba 21), katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Azam FC itakuwa mgeni wa mchezo huo, huku ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kuondolewa kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Akhdar ya Libya.

Afisa Habari wa muda wa Azam FC Hashim Ibwe amesema Mshambuliaji Sopu aliyepata majeraha ya misuli ya paja bado yupo chini ya uangalizi wa kimatibabu, hivyo atakosa mchezo wa kesho dhidi ya KMC FC.

Amesema Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Coastal Union ya Tanzania amekosa sehemu ya maandalizi ya mchezo huo, kutokana na hali yake, lakini Benchi la Ufundi linaamini wachezaji waliosalia kikosini wataikamilisha kazi itakayowapeleka Uwanja wa ugenini.

“Kwa wachezaji ambao wataukosa mchezo dhidi ya KMC FC ni Abdul Sopu ambaye yupo kwenye uangalizi maalum kwa kuwa alipata maumuvu tulipocheza dhidi ya Al Akhdar Jumapili (Oktoba 16) Uwanja kwenye Azam Complex- Chamazi.” amesema Ibwe

Kuhusu matarajio yao kuelekea mchezo wa kesho, Ibwe amesema wanatarajia kupata upinzani kutoka kwa wenyeji wao, lakini wanaamini matokeo mazuri yatakua upande wao, kutokana na kuwa na kikosi Bora na Imara tofauti na KMC FC.

“Tunategemea kupata upinzani kutoka kwa KMC FC, lakini dhamira yetu kuu kwenye mchezo huo ni kupata ushindi dhidi yao, mchezo huu unakuja baada ya sisi kutolewa kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo tuna hamu ya kurejesha furaha ya ushindi,”

“Tunawaheshimu KMC FC kwa sababu ni klabu inayoshiriki Ligi Kuu, tunajua wana kikosi kizuri, lakini sisi tuna kikosi Kizuri, Imara na Bora zaidi yao, tunaamini mambo yatatunyookea kesho Uwanja wa Uhuru.” amesema

Azam FC inakwenda kucheza uwanja wa ugenini ikiwa imeshajikusanyia alama 11 zinazoiweka nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku wenyeji wao wakiwa na alama 10 zikiwaweka nafasi ya sita.

Mayele: Tunajua tutaifanya nini Simba SC
Phiri, Chama waandaliwa kuivuruga Young Africans