Wakati Young Africans ikitamba wanasikia raha sana wanapomfunga mtani wao Simba SC, Kaimu Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Juma Mgunda, amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa keshokutwa Jumapili (Oktoba 23) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mgunda, ambaye itakuwa ni ‘dabi’ yake ya kwanza tangu ajiunge na Simba SC mwanzoni mwa mwezi Septemba, amekiri mchezo huo utakuwa ngumu, lakini kikosi chake kipo kamili kwa ajili ya kupambana.
Mgunda amesema kikosi chake kiko tayari kumaliza ‘ubabe’ dhidi ya watani zao na kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi hiyo inayodhaminiwa na Benki ya NBC.
“Nikiri hii itakuwa ‘dabi’ yangu ya kwanza nikiwa Kocha wa Simba, changamoto ya michezo hii hakuna mtu asiyejua, timu hizi zinapokutana basi heka heka inakuwa kubwa.”
“Naamini kikosi nilichonacho nikiri utakuwa mchezo mkubwa, mgumu na wenye ushindani, haijalishi matokeo yaliyopita ya timu yoyote ile.”
“Kwa kawaida mchezo huu huwa una shughuli, niseme tu najiandaa vizuri na hiyo shughuli ya Jumapili, vijana wenyewe wanaelewa mchezo huu una uzito gani na wanatakiwa wafanye nini na hata mashabiki wetu wana matumaini makubwa,” amesema Mgunda
Kocha huyo ameongeza maandalizi yote muhimu yamekamilika na kilichobakia ni kuwaaminisha wachezaji wake wanaweza kama walivyofanya kwenye michezo ya kimataifa iliyopita.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Agosti 13, mwaka huu katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Young Africans ilichomoza na ushindi wa mabao 2-1.
Simba yenye alama 13 sawa na Young Africans, ndio kinara wa ligi hiyo lakini ikiwa na moto baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.