Klabu ya Simba SC imejizatiti kupambana vilivyo ili kurejesha furaha kwa Mashabiki na Wanachama wake, kupitia mchezo wa keshokutwa Alhamis (Oktoba 27), dhidi ya Azam FC.
Simba SC itakuwa mgeni katika mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare ya 1-1 walioipata dhidi ya Young Africans juzi Jumapili (Oktoba 23).
Azam FC wao walipoteza dhidi ya KMC FC kwa kufungwa 2-1 siku ya Ijumaa (Oktoba 21, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Meneja wa Habari na Mawasilino Ahmed Ally amesema kikosi chao kimeshaanza maandalizi ya mchezo huo, wakiwa na matumaini makubwa ya kurejesha furaha kwa Mashabiki na Wanachama wao, ambao wamezoea kufurahi.
Amesema matokeo ya sare walioyapata dhidi ya Young Africans yamewapa hasira, hivyo watahakikisha wanapambana kwa malengo makubwa dhidi ya Azam FC, ili kupata matokeo ambayo yatawapoza.
“Tuna hasira sana na matokeo ya sare tulioyapata dhidi ya Young Africans, tunakwenda kucheza dhidi ya Azam FC, hawa jamaa watakua na kazi kubwa sana kwa sababu mioyo yetu imekunjamana kwa hasira ya kilichotokea juzi Jumapili,”
“Tunakiri Azam FC wana timu nzuri na tunaamini watatupa upijzni mzuri, lakini tunasisitiza hasira zetu zipo pale pale kwa sababu hatutaki utani katika Ligi ya msimu huu, tutapambana ili kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huu.” amesema Ahmed Ally
Kabla ya kucheza dhidi ya Young Africans, Simba SC ilidumisha furaha kwa Mashabiki na Wanachama wake kwa kupata ushindi Nyumbani na Ugenini katika Michuano ya Kimataifa (Ligi ya Mabingwa Barani Afrika), dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola.
Simba SC inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 14 sawa na Young Africans na Singida Big Stars, lakini klabu hiyo ya Msimbazi ina uwiyano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.