Kaimu Kocha Mkuu wa Azam FC Kalimangonga Ramadhan Mtoro Ongala, amefunguka kwa mara ya kwanza tangu alipokabidhiwa jukumu la kukiongoza kikosi cha ‘Wababe wa Chamazi’.
Kali aliyewahi kucheza Azam FC na Young Africans alikabidhiwa jukumu hilo kwa kusaidiwa na Mchezaji Mkongwe Agrey Morris, baada ya kutimuliwa kwa Kocha kutoka nchini Ufaransa Denis Lavagne.
Ongala amesema ana uhakika timu itafanya vizuri katika mchezo ujao dhidi ya Simba SC na michezo mingine, kwa kuwa kikosi chake kimesheheni wachezaji wazuri na wenye uwezo wa kupambana na yoyote kwenye Ligi ya Tanzania Bara.
“Yawezekana mfumo wa mwalimu aliyepita ulikuwa mgumu au kuna sababu nyingine ya kupata matokeo yaliyoridhisha. Wachezaji wote wana uwezo, na ndio maana tulifanya vizuri katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, japo hatukufanikiwa kusonga mbele.” amesema Kaimu Kocha Mkuu wa Azam FC Kally Ongala
Kocha huyo alianza kukinoa kikosi chake juzi Jumapili (Oktoba 23) kwa ajili ya kujiwinda na mchezo dhidi ya Simba SC, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.