Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, umekanusha taarifa za kuwa mbioni kumtimua Kocha Nasreddine Nabi, kama ilivyoripotiwa mapema leo Jumatano katika Gazeti la Mwanaspoti.

Kwa mujibu wa taarifa za Gazeti hilo, Uongozi wa Young Africans unadaiwa kuwa kwenye mpango wa kusitisha ajira ya Kocha huyo kutoka nchini Tunisia na nafasi yake itajazwa na Kocha wa Mabingwa wa Uganda Vipers SC, Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo.

Young Africans imetoa Taarifa kwa Umma kupitia APP ya klabu hiyo ikikanusha taarifa hizo, kwa kusisitiza Nabi bado ni Kocha Mkuu wa kikosi chao.

Taarifa hiyo inaeleza: UONGOZI wa Yanga unapenda kuwataarifu mashabiki na Wanachama wake kuwa Nasreddin Nabi, bado ni kocha mkuu wa timu yetu.

Nabi alijiunga na Yanga April, 2021 na amekuwa na rekodi nzuri ya kuiongoza timu yetu kubeba Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, bila kupoteza.

Akizungumza na YANGA MEDIA, Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine amewaomba mashabiki na wanachama wa Yanga kufatilia taarifa za uhakika za timu yao kupitia vyanzo rasmi vya habari vya klabu.

“Niwaombe mashabiki na wanachama wetu kuwa na utaratibu wa kufatilia taarifa za klabu yetu kutoka kwenye vyanzo vyetu vya habari.

“Tuna YANGA APP. Tuna Website ya Young Africans na kurasa zetu za mitandao ya kijamii ambazo zimekuwa zikitoa taarifa za klabu yetu na kwa wakati sahihi,” alisema Andre.

Uongozi unamtakia kila la kheri kocha Nabi na benchi lake la ufundi kwenye maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya KMC utakaopigwa saa 1:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Waziri Mkuu atembelea kiwanda kinachotengeneza mabehewa ya TRC
Nabi akata mzizi wa FITNA, azungumza hadharani