Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo na kasi ya ujenzi wa mabehewa mapya kwa ajili Reli ya Kisasa (SGR) ya Shirika la Reli Tanzania yanayotengenezwa na kampuni ya Sung Shin Rolling Stock (SSRT) iliyoko nchini Korea Kusini.

Majaliwa ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2022 mara baada ya kutembelea kampuni ya SSRST inayotengeneza mabehewa na injini za treni nchini Korea Kusini.

“Kati ya mabehewa 81 ambayo Tanzania inatengeneza kutoka kwenu, tayari 36 yamekamilika na yameshapelekwa nchini Tanzania na 45 yaliyobaki yanategemewa kukamilika Machi, 2023. Mabehewa haya ni ya daraja la tatu na yatatoa huduma zote muhimu.” Amesema Majaliwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu amemkaribisha nchini Rais wa Kampuni hiyo Gye Shul Park aje kuwekeza nchini Tanzania kutokana na fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo mpango wa Serikali wa kuendelea kuiboresha sekta ya usafiri wa reli.

“Mnakiwanda kikubwa, teknolojia ya hali ya juu pamoja na utaalamu na watalaam kwenye eneo hili. Kwa sasa tuna mipango mikubwa ya kuendelea kuiboresha sekta hii ya usafiri wa reli, yapo maeneo tofauti kwenye mpango wa kuunganishwa na reli ya kisasa (SGR), nakukaribisha kuja kuwekeza kitu kama hiki Tanzania.” 

Aidha, Majaliwa alitembelea kituo cha Seamul Undong  ambacho ni taswira ya maendeleo ya Korea kupitia mpango wa kuviwezesha vijiji ambao unatekeleza mpango huo nchini Tanzania katika mkoa wa Morogoro (Pangawe) na Zanzibar.

Waziri Mkuu, alimshukuru Rais wa Kituo hicho na kumuomba kuendelea kutoa ushirikiano ili kukuza zaidi mpango huo na kufikia maeneo mengi zaidi.

“Mfumo huu kwasasa umekuwa wa kitaifa, ushirikishwaji wa Wananchi ni mkubwa, sasa tunataka tuikuze zaidi, haya maeneo ya Morogoro na Zanzibar tunataka yawe mifano, kwenye utekelezaji wa eneo hili”.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 26, 2022   
Young Africans yalikana MWANASPOTI