Klabu ya Geita Gold FC imejinasibu kuwa tayari kwa mchezo wa kesho Jumamosi (Oktoba 29) wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mabingwa Watetezi Young Africans.

Miamba hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara itapapatuana katika Uwanja wa CCM Kirumba kuanzia mishale ya saa kumi jioni, huku kila upande ukiwa na hamu ya kuzinasa alama tatu za mchezo huo.

Kaimu Katibu Mkuu wa Geita Gold, Liberatus Pastory amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika huku akisema kikosi chao kimeshatia nanga jijini Mwanza baada ya mchezo wa Ligi dhidi ya Ruvu Shooting uliochezwa juzi Jumatano (Oktoba 26).

Amesema ili kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mtanange huo wachezaji wameahidiwa motisha ambayo hakuweka wazi ni ya namna gani lakini akasisitiza itakuwepo na wachezaji wanaitambua kwani wamedhamiria kuisimamisha Young Africans na kuvunja rekodi ya kucheza michezo 44 ya Ligi bila kufungwa.

“Tumejiandaa kwa mchezo huu, tuna uhakika tutakuwa na mchezo mzuri na kupata matokeo kama ambavyo imekuwa katika Mechi zetu nne zilizopita, tuna imani sisi ndiyo tutasitisha rekodi ya Young Africans kutofungwa kwenye ligi wachezaji waendelee kujituma kwa spirit na nguvu ile ili tuweze kutimiza malengo yetu,”

“Kama ilivyokuwa kwenye mchezo na Simba motisha ipo na vijana wanafahamu lakini hatuwezi kuiweka wazi kwamba ni motisha ya namna gani. Kama ilivyokuwa msimu uliopita tulilenga nafasi tano safari hii tunataka nafasi tatu za juu,” amesema Pastory ambaye pia ni mjumbe wa kamati tendaji ya klabu hiyo.

Geita Gold FC inakwenda kukutana na Young Africans ikiwa nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na alama 13, ikishinda michezo mitatu, ikipoteza miwili na kutoka sare miwili.

Simba Queens yaivutia kasi AS FAR Queens
Parimatch yafanya maboresho, yaja kibabe na mfumo mpya