Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada ameitaka jamii nchini kushiriki shughuli mbalimbali za kimaendeleo kwa kupanda miti, ili kuendeleza ustawishaji wa mazingira kwa manufaa ya Taifa na mtu moja mmoja.
Ngwada ameyasema hayo, wakati akifanya mahojiano na Dar24 ofisini kwake hivi karibuni na kusema wito huo unatokana na ukweli kuwa Dunia imekumbwa na mabadiliko yahali ya hewa ambayo yanahitaji kukabiliwa kwa njia mbalimbali ambazo zitasaidia kuepusha madhara zaidi.
Amesema, “Sote tunatambua kuwa mabadiliko ya tabia nchi yameathiri mambo mbalimbali ikiwemo suala la mazingira, na kibaya zaidi maeneo mengi yameathiria na ukame lakini wana Iringa tunayo nafasi ya kufanya mapinduzi, tupande miti.”
Aidha, Meya Ngwada ameongeza kuwa suala la upandaji miti liwe ni sehemu ya maisha ya kila mmoja, kwani lisaidia kuleta tija kwa Taifa na vizazi vijavyo na kwamba pamoja na Serikali kuweka msisitizo juu ya suala hilo, pia jamii inatakiwa kuhamasishana katika ustawishaji na utunzaji wa mazingira.
Hata hivyo, Ngwada amesema mkoa huo umekuwa kinara katika shughuli za uhifadhi wa mazingira, na kwamba watahakikisha wanaendelea kuitetea nafasi yao kwa kujibidiiisha kwenye upandaji wa miti na kuisisitiza jamii juu ya umuhimu wa suala hilo ili Manispaa hiyo iwe mfano wa kuigwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, inavivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo jiwe la Gangilonga, boma na Soko la Mjerumani ambapo wakazi wake hufaidika kwa kuongoza watalii wa ndani na nje kujionea na kupata historia ya maeneo hayo.