Rwanda imemshutumu jirani yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuchochea wasiwasi baina yao baada ya Kongo hapo jana (Oktoba 30, 2022), kumuagiza balozi wa Rwanda kuondoka nchini humo katika kipindi cha masaa 48.
Hatua hiyo, inafuatia kuongezeka kwa mashambulizi ya uasi mashariki mwa Kongo, wakati taifa hilo likiamini kwamba Rwanda inawasaidia waasi wa M23 wanaozidi kujiimarisha kwenye eneo hilo tangu mwaka uliopita.
Baada ya Balozi Vincent Karega kufukuzwa, Rwanda imesema inasikitishwa kuona Kongo inaendelea kuifanya nchi yake kama mbuzi wa kafara, ili kuficha na kuvuruga udhaifu wake kiutawala, na kuongeza kuwa vikosi vyake vilivyoko mpakani vinasalia katika tahadhari.
Kundi la M23, limekuwa kiini cha mvutano baina ya mataifa hayo mawili, na usiku wa jana (Oktoba 30, 2022), Umoja wa Afrika, AU ulisema una wasiwasi mkubwa kutokana na kutetereka kwa hali ya usalama katika eneo hilo, la mashariki mwa Kongo.