Mshambuliaji kutoka DR Congo na Klabu ya Young Africans Fiston Kalala Mayele amejitoa muhanga kuelekea mchezo wa Mtoano Kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo wa Mkondo wa Kwanza utakaopigwa Keshokutwa Jumatano (Novemba 02) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mshambulaiji huyo amesema wapo tayari kwa mchezo dhidi ya Club Africain, na watahakikisha wanapambana ili kushinda mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Soka nchini Tanzania na wale wa Tunisia.
Mayele amesema kwenye mchezo huo wa Mkondo wa Kwanza, Young Africans inapaswa kushinda idadi kubwa ya mabao katika Uwanja wake wa nyumbani, ili wasirudie makosa walioyafanya kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
“Tunatakiwa kufunga mabao mengi, pia tusiwaruhusu kupata bao hapa nyumbani, hii inahitaji umakini mkubwa, lakini tutahakikisha tunafanikisha hayo yote katika mchezo wa hapa nyumbani,”
“Tunajua makocha wetu wanawajua vizuri kwa kuwa wametoka huko Tunisia, kitu ambacho kinaweza kututofautisha sisi na wao ni kwamba timu yetu imeshacheza michezo mikubwa ya ushindani kuanzia Ligi na Kimataifa, wao Ligi yao haijaanza kwa hiyo tunatakiwa kutumia nafasi hii vizuri.”
“Hii ni nafasi kubwa iliyosalia kwetu na kulinda heshima ya Young Africans baada ya kutolewa na Al Hilal, tunatakiwa kuhakikisha tunashinda vizuri hapa nyumbani.”
“Tunatambua utakua mchezo mgumu kwa kuwa wapinzani wetu ni klabu kongwe, kila kitu kwetu kinawezekana kama tukijipanga sawasawa nawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi Uwanjani siku ya mchezo.” amesema Mayele
Young Africans iliangukia Hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa na Al Hilal jumla ya mabao 2-1.
Kwa upande wa Club Africain ambayo tayari imeshawasili jijini Dar es salaam, ilitinga hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho baada ya kuibamiza Kipanga FC ya Zanzibar mabao 7-0.