Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema Kikosi chake kina kazi kubwa ya kuhakikisha kinakusanya alama za kutosha mwezi Novemba, ambao watakabiliwa na Michezo sita ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika michezo hiyo sita, Simba itaanza kucheza dhidi ya Singida Big Stars katika Uwanja wa Liti mkoani Singida Novemba 9 kabla ya siku tatu baadaye kurejea Dar es Salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikaribisha Ihefu FC.
Novemba 16, Simba itashuka tena katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuialika Namungo FC na siku tatu baadaye itakuwa ugenini kuvaana na Ruvu Shooting kabla ya Novemba 23 kuifuata Mbeya City katika Dimba la Sokoine jijini Mbeya.
Mchezo wa mwisho mwezi huu kwa Simba, utakuwa dhidi ya Polisi Tanzania ugenini utakaopigwa Novemba 27, ambao utakamilisha hesabu zao hizo.
Kocha Mgunda amesema malengo yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika kila mechi ili kufikia kile kinachotarajiwa na Wanasimba.
Amesema anajua hakuna mechi rahisi kwao na ushindani umekuwa mkubwa kwenye ligi, hivyo yeye na wachezaji wake wanalazimika kupambana bila kuchoka ili kufikia kile ambacho wamekikusudia.
“Hakuna mechi rahisi, tunatakiwa kujipanga vizuri katika mechi zote tutakazocheza mwezi huu [Novemba] ili kutimiza lengo letu, kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kutimiza wajibu wake, naamini tukifanya hivyo uhakika wa ubingwa msimu huu ni mkubwa,” amesema Mgunda.
Kwa sasa Simba SC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama 17 katika michezo nane, wakizidiwa alama tatu na watani wao wa jadi, Young Africans walioko kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.