Maafisa watatu wa Marekani wamesema wamezungumza na Saudi Arabia kuhusu taarifa za ujasusi za Iran kuwa huenda ikawa inapanga mashambulizi dhidi ya taifa hilo la kiarabu, taarifa ambazo zinakuja wakati serikali ya rais Joe Biden ikiendelea kuikosoa Iran kwa namna inavyowakamata waandamanaji na kuikosoa pia kutuma ndege zisizokuwa na rubani nchini Urusi zinazotumika katika vita vyake na Ukraine.
Baraza la usalama la kitaifa limesema lina wasiwasi juu ya kitisho hicho na linaendelea kuwa na mawasiliano ya kijeshi na kijasusi na Saudi Arabia. Baraza hilo limeongeza kuwa halitojiuzuia kuchukua hatua kulinda masilahi yake na washirika wake katika kanda hiyo huku Marekani ikitangaza kujaribu kuiondoa Iran kutoka katika bodi ya Umoja wa Mataifa inayopambana kutaka uwepo wa usawa wa kijinsia.
Marekani imesema imechukua uamuzi huo kutokana na Iran kuendelea kukiuka haki za wanawake na wasichana, katika kamata kamata yake dhidi ya waandamanaji waliomiminika barabarani, tangu mwezi Septemba baada ya kifo cha msichana wa miaka 22 Mahsa Amini, kilichotokea baada ya kukamatwa na polisi wa maadili nchini humo.
Makamu wa rais wa Marekani, Kamala Harris alitangaza hatua hiyo ya Marekani kufanya kazi na mataifa mengine, kuiondoa Iran katika kamisheni hiyo akisema taifa lolote linalokiuka haki za wanawake, halipaswi kuwa na jukumu ndani ya shirika lolote la Kimataifa lililo na jukumu la kulinda haki hizo.