Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara za Maji, Mifugo na Uvuvi na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mifugo kuhakikisha miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa kwenye maeneo yenye shughuli za wafugaji inafanyiwa tathimini na kupewa kipaumbele cha kutengeneza miundombinu kwa ajili ya mifugo.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Novemba 3, 2022 Bungeni jijini Dodoma, na kuongeza kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo kwa ajili ya mifugo unatakiwa kuendana na utengenezaji wa maeneo ya kunyweshea, badala ya kuiacha mifugo kwenda kwenye mabonde ya hifadhi.
Hata hivyo, ametoa maagizo matatu kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA), ya kukabiliana na changamoto ya moto kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo Mlima Kilimanjaro pale yanapojitokeza majanga ya ina mbalimbali.
Amesema, ’’Hakikisheni mnaunda kitengo ndani ya TANAPA cha kukabiliana na majanga au maafa yanayotokea ndani ya hifadhi. Pia wekezeni kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa hususan katika tahadhari, utambuzi na uzimaji moto pamoja na kuimarisha shughuli za doria na uokoaji kwa kushirikisha jamii na wadau.’’