Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), limesema kuna ulazima wa bara la Ulaya kuchukua hatua za haraka za kuzuia ukosefu wa gesi asilia kwa mwaka ujao (2023), wakati Urusi ikiendelea kupunguza utoaji wa gesi hiyo kwa mataifa ya Ulaya, kufuatia vita vyake na Ukraine.
IEA yenye na makao yake makuu jijini Paris nchini Ufaransa, imesema Ulaya inaweza kukosa kiwango cha mita za ujazo bilioni 30 inachohitaji kwa ajili ya kuinua uchumi wake, na kujaza maeneo ya uhifadhi wa gesi wakati wa kipindi cha kiangazi mwaka 2023.
Taarifa hiyo ya IEA imezidi kueleza kuwa, hatua hiyo itaharibu maandalizi ya kipindi cha baridi cha mwaka 2023 na 2024 na hivyo kuwepo kwa uwezekano wa shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii zinazotegemea nishati ya gesi kudorora.
Serikali ya nchi ya Urusi, ilikata ghafla usambazaji wa gesi kwa Ulaya ikiwa ni hatua ya kujibu vikwazo ilivyowekewa na Mataifa ya Magharibi, kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine ambapo Bara hilo limefanikiwa kujaza maeneo yake ya uhifadhi wa gesi, katika kipindi hiki cha baridi.