Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Injinia Hersi Said amekerwa na tabia ya baadhi ya watu wasiotakia mema klabu hiyo, kwa kutumia kauli yake aliyoitoa jijini Mwanza mwishoni mwa juma lililopita alipozungumza na Wanachama.
Hersi Said ameonyesha kukerwa na hilo, alipozungumza na Wanachama na Mashabiki wa Young Africans kupitia Yanga TV jana Alhamis (Novemba 03), kuhusu mambo mbalimbali ya klabu hiyo.
Kiongozi huyo amesema watu hao wasioitakia mema klabu ya Young Africans wamekua wakitumia vibaya sehemu ya Picha za Video za mkutano wake na Wanachama wa Young Africans Mwanza, hasa pale aliposema “Watu wameshakula mihogo huko wanasema wameumizwa na Matokeo”.
“Wapo Baadhi ya Watu wasioitakia mema klabu yetu wametumia kauli yangu ambayo nilitumia wakati nazungumza na viongozi wa matawi mkoani Mwanza wakiitumia kauli ile kuwakejeli mashabiki wa Timu yetu.
“Nataka niwahakikishie uongozi wenu ni uongozi ambao ni sikivu sana lakini umekuwa karibu na wanachama wa kila aina nikiwemo mimi kama Kiongozi wa klabu hii, nimekuwa nikifika katika kila aina ya maeneo ikiwemo maeneo ya watu wenye uhitaji sana. Na nimekuwa nikisikiliza na kuheshimu watu wa aina zote”
“Naomba wanachama na wapenzi wa Young Africans wapuuze kejeli zinazotumia sura yangu katika kuonesha kejeli hizo kwa wanachama.” amesema Injinia Hersi Said.
Kejeli na matumizi mabaya ya Kauli ya ‘Wala Mihogo’ imekuja baada ya Young Africans kuambulia sare ya 0-0 dhidi ya Club Africain kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika.