Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhandisi Ezra Chiwelesa, ameliomba Bunge kuielekeza serikali kuondoa miradi ya ujenzi wa njia za kuruka na kutua ndege chini ya wakala wa barabara nchini (Tanroads), huku akionya hatari ya kushindwa kuhimili vigezo vinavyowekwa na mamlaka za kimataifa.
Ameyasema hayo, wakati akichangia hoja ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2021.
“Tanroads wametusababishia matumizi mabaya ya fedha za umma kwa takribani Shilingi bilion 68.73 katika mwaka wa fedha 2021 kama riba kwa kuchelewesha malipo,” amesema Chiwelese.
“Mbaya zaidi Tanroads wameendelea kugawa miradi kwa wakandarasi wa kigeni ambao wamekuwa wakiwatoza riba.”
Kwa mujibu wa Chiwelesa, amesema miradi ya ujenzi wa njia za kuruka ndege inafaa iwe chini ya mamlaka ya viwanja vya ndege hata hivyo Tanroads imepewa upendeleo na serikali kusimamia ujenzi wa barabara, madaraja na njia za ndege.
Mhandisi Chiwelese amesema kuwa kuna viwango ambavyo vinapaswa kuzingatiwa katika ujenzi wa njia za kuruka ndege ikiwa ni pamoja na majengo.
Mhandisi Chiwelesa amesema wakati wa mjadala bungeni mjini Dodoma kuwa ripoti ya Kamati ya Bunge ya PAC imeonesha Tanroads hawana Bodi kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Vilevile, Bodi ya Tanroads ni ya washauri na sio Wakurugenzi hivyo kuna hatari ya kuendelea kuona hasara katika Wakala wa Barabara Nchini.
Kiasi cha Sh bilioni 68.7 ambacho Tanroads imelazimika kulipa mwaka jana kinatosha kujenga kilometa 68 za lami.