Simba imeendelea kujifua kwenye katika uwanja wake wa Mo Simba Arena uliopo Bunju, Dar es Salaam, kwa ajili ya mechi zijazo za Ligi Kuu ikiwemo ile ya Novemba 9 dhidi ya Singida Big Stars.

Ushindi wa mabao 5-0 ilioupata dhidi ya Mtibwa Sugar uliongeza mzuka kwa nyota wake, viongozi, mashabiki na benchi la ufundi chini ya kocha Juma Mgunda aliyetenga siku tano maalumu za kukinoa kikosi chake ili kuhakisha kinakwenda kuifunga Singida.

Siku hizo tano zilianza kwenye mazoezi ya jana na kuendelea na benchi la ufundi linaamini zitatosha kumaliza mchezo kabla ya kusafiri kwenda Singida kucheza dakika 90 zitakazoamua matokeo.

Mgunda anayesifika kwa soka la kisasa la pasi nyingi na kasi alitumia muda wake wa mapumziko mafupi ya siku mbili baada ya mechi na Mtibwa, kuisoma Singida namna inavyocheza na jinsi gani ya kuikabili na kinachofuata ni kuwapa mbinu wachezaji wake za kushinda mechi hiyo.

“Nimewaona Singida, ni timu nzuri yenye wachezaji bora na wenye uzoefu wa kutosha, nadhani itakuwa ni mechi yenye ushindani kwetu.”

“Mwisho wa mechi ndo mwanzo wa mechi nyingine, baada ya kumalizana na Mtibwa, mimi na wenzangu tulianza hapo hapo maandalizi dhidi ya Singida tunataka kuandaa timu tukiwa Dar es Salaam na ndani ya siku tano nadhani tutakuwa tumeshajua tunaindiaje katika mechi hiyo,” amesema Mgunda.

Katika maandalizi ya mechi hiyo, Simba itakuwa na wachezaji wake wote, baada ya kurejea kwa viungo, Sadio Kanoute na Victor Akpan, mabeki Shomari Kapombe, Israel Mwenda na Mohammed Ouattara na mshambuliaji Jimmyson Mwanuke waliokuwa Majeruhi.

Mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Liti, ni wa kwanza kuzikutanisha timu hizo, kwani msimu huu ni wa kwanza kwa Singida kwenye Ligi Kuu baada ya kupanda ikitokea Championship (zamani Daraja la Kwanza) ilikokuwa inaitwa DTB kabla ya kubadilishwa jina.

Wakati Simba ikitamba na ubora wa kikosi chake kilichojaa nyota wengi, hasa eneo la ushambuliaji ambalo ni hatari, Singida pia ina wakali kibao wenye ubora wa hali ya juu, jambo litakalofanya mechi hiyo kuwa na mvuto.

Mzamiru Yassin mchezaji bora Simba SC
Marubani kuanza mgomo shinikizo la madai