Karibu waumini 30,000 wamehudhuria ibada ya wazi iliyoongozwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis nchini Bahrain ikijumuisha pia maandamano madogo ya ndugu wa wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo.
Kiongozi huyo, ambaye hakusimama kuzungumza na waandamanaji hao alipokelewa kwa densi na mauwa ndani ya shule ya Sacred Heart mjini Manama, ambako aliwahimiza watoto kukumbatia utamaduni wa kuwajali wengine.
Papa Francis, yuko kwenye ziara yake ya pili katika kanda ya ghuba iliyo na idadi kubwa ya Waislamu, ambayo pia ni nyumbani kwa mamilioni ya wafanyakazi wa kigeni, wakiwemo Wakatoliki.
Hata hivyo, wakati ziara yake imejikita katika mdahalo na Uislamu, imeshuhudia pia kutolewa kwa shutuma za ukiukaji wa haki za binadamu katika kanda hiyo ya ghuba.