Maafisa wa jeshi nchini Somalia, wamesema watu watano wameuawa na wengine 11 kujeruhiwa wakati mshambuliaji wa kujitolea muhanga alipojiripuwa kwenye lango la mbele la kambi ya mafunzo ya kijeshi ya Jenerali Dhaga-Badan mjini Mogadishu.
Mkuu wa jeshi la Somalia, Jenerali Odawa Yusuf ameliambia shirika la habari la serikali ya nchi hiyo kuwa mshambuliaji huyo, alikuwa akijifanya kuwa mmoja wa maafisa waliokuwa wakipata mafunzo katika kambi hiyo iliyoko wilayani Wadajir.
Afisa wa kijeshi, Abdirahman Ali, ameambia shirika la habari la Associated Press kwamba waliouawa ni raia waliokuwa wakitembea barabarani na maafisa waliokuwa wanapata mafunzo hayo.
Tyari kundi la al-Shabab limedai kuhusika na shambulizi hilo, ambalo imelengwa mara kadhaa katika siku za nyuma katika eneo lililo karibu na kambi kubwa ya jeshi la Uturuki, nchini Somalia.