Uongozi wa Simba SC umeweka wazi kuwa mwishoni mwa mwezi huu Novemba utakamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa uzio kwenye Viwanja vyao vya Bunju, kisha kuanza utekelezaji wa mkakati mzito wa awamu ya pili na ile ya mwisho ambayo itahusisha ujenzio wa Hostel, Gym pamoja na viwanja ikiwemo Uwanja mkubwa zaidi wa kucheza michezo ya ushindani.
Juzi Jumamosi (Novemba 05) Kamati ya ujenzi ya mradi huo ilitembele Uwanja wa Bunju ‘ Mo Simba Arena’ kwa ajili ya kukagua maendeleo na kuweka wazi kuwa mpaka sasa wamekamilisha asilimia 70 ya mpango kazi wao wa awamu ya kwanza.
Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Crescentius Magori alisema: “Mradi huu kama ambavyo tuliuelezea mwanzo, ni mradi mkubwa ambao unakwenda kuibadilisha Simba SC kuwa miongoni mwa timu zenye nguvu Afrika, sio tu Uwanja bali kwenye miundombinu na uchumi.”
“Mwishoni mwa mwezi huu Novemba tunatarajia kumaliza awamu ya kwanza ya ujenzi wa uzio ambao umefikia asilimia 70 na mara tu tutakapokamilisha basi tutatangaza awamu ya pili ambayo itahusisha miundombinu kama hosteli, Gym na maboresho ya viwanja vya mazoezi kabla ya awamu ya mwisho ambayo itahusisha ujenzi wa uwanja mkubwa wa kucheza michezo ya ushindani.” amesema Magori