Kocha Mkuu wa Simba Queens Charles Lukula, amesema hana cha ziada zaidi ya kumshukuru Mungu kwa kufanikisha malengo ya kikosi chake kucheza Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa Wanawake.
Simba Queens ilijihakikishi kucheza hatua hiyo juzi Jumamosi (Novemba 5), kwa kuibanjua Green Buffaloes ya Zambia 2-0, na kufikisha alama 6 zinazoiweka katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi A.
Lukula amesema baada ya kumaliza dakika 45 za kwanza bila kupata bao, alitumia muda wa mapumziko kuwaambia wachezaji wake waongeze juhudi kwenye kushambulia ili wafunge magoli na hatimaye kupata ushindi.
Kocha huyo kutoka nchini Uganda mesema mabadiliko aliyofanya ya kumwingiza Asha Djafari na Vivian Corazone Odhiambo yalisaidia kuongeza nguvu katika kikosi chake na hatimaye kupata mabao mawili yaliyowafanya wasonge mbele kwenye michuano hiyo.
“Napenda kumshukuru Mungu, wachezaji, viongozi wote wa Simba na mashabiki, tumekuja kuchukua kikombe, tutaendelea kupambana kuhakikisha tunafikia malengo, uwezo na nia ya kuleta heshima tunayo,” amesema kocha huyo.
Ameongeza kuwa anafurahi pia kuona amekuwa Mganda wa kwanza kuipeleka timu katika hatua hiyo na anawashukuru Simba kwa kumpa nafasi ya kuiongoza timu kufika hatua hiyo kwenye fainali hizo.
Oppa Clement, nahodha wa Simba Queens, alianza kwa kuwashukuru mashabiki wa klabu hiyo kutokana na sapoti ambayo wamewapa kuanzia mwanzo wa mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya pili barani hapa.
“Asanteni sana mashabiki wa Simba, asante sana, tumekuja kupambana na tunaahidi kuendelea kuipambania timu yetu, tunajua kila kitu ni hatua,” alisema mshambuliaji huyo wa Timu ya Soka ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars.
Fainali za mashindano hayo zitafanyika Novemba 13, mwaka huu jijini Rabat na bingwa atajinyakulia kitita cha Dola za Marekani 400,000 sawa na Sh. milioni 930.9, wakati mshindi wa pili atajinyakulia zawadi ya Dola za Marekani 250,000 ambazo ni sawa na Sh. milioni 581.8.