Baada ya Kocha Mkuu wa Young Africans, Nasreddine Mohamed Nabi, kuhakikisha kikosi chake kinakuwa salama katika kambi yake ya siku tatu iliyoweka mjini Sousse ambapo ndipo nyumbani kwake, mwalimu huyo sasa atakiongoza kikosi hicho kesho Jumanne (Novemba 08), kuelekea jijini Tunis utakapopigwa mchezo wa mkondo wa pili ya mchujo dhidi ya Club Africain kuwania kufuzu Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kikosi cha Young Africans kilitua Sousse ambako ndio nyumbani kwa Nabi, tangu Jumamosi (Novemba 05) kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Olympique Hamadi Agrebi jijini Tunis, ambapo ni umbali wa takriban Km. 140 kutoka walipo.

Kikosi hicho kimejichimba katika mji wa Sousse chini ya Nabi kikijifua vikali mara mbili kwa siku, asubuhi na jioni lengo likiwa ni kuhakikisha kinapata matokeo mazuri na kusonga mbele hatua ya makundi baada ya kupoteza nafasi kama hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kutolewa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.

Nabi amesema anaifahamu timu ya Club Africain inapokuwa nyumbani tofauti na walivyocheza ugenini katika mechi yao ya kwanza.

Amesema kila mchezaji anatakiwa kuwa makini na kufanya majukumu yake kwa kuzingatia vitu muhimu anavyowapa mazoezini hasa kuongeza umakini kwenye mipira ya faulo kutokana na ubora wa Club Africain katika idara hiyo.

“Hatutaki kuruhusu wapate bao katika mipira hiyo ya adhabu, lakini mabeki kuwa makini zaidi na washambuliaji wa Club Africain kwa sababu mechi yao ya mwisho nyumbani walishinda mabao 7-0 dhidi ya Kipanga.”

“Katika mchezo huo walifunguka kwa sababu wako nyumbani, ugenini hawakucheza hivyo, kwa kuwa tumeona ubora wao hatutakiwi kuwapa nafasi ya kufunguka na tunafanyia kazi kwa ajili ya kuwa imara zaidi,” amesema Nabi.

Amesema mchezo hautakuwa rahisi na hawatacheza kwa sababu ya historia bali amewataka wachezaji kila mmoja kupambana kwa ajili ya kwenda kutafuta matokeo mazuri katika mchezo huo.

Katika mchezo huo, Young Africans inahitaji sare yoyote ya mabao ama ushindi ili kufuzu na kama matokeo yatakuwa suluhu, basi changamoto ya mikwaju ya penalti itachukua nafasi yake, hiyo ikitokana na sare tasa timu hizo zilipokutana Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumatano iliyopita (Novemba 02).

Timu itakayofuzu itasubiri kujua wapinzani wake watatu kwenye hatua ya makundi wakati Droo itakapochezeshwa Novemba 16, mwaka huu jijini Cairo, Misri yalipo makao makuu ya CAF.

Wavunja rekodi kukamatwa na Bangi tani 32
Liverpool mdomoni mwa mabingwa Ulaya