Kikosi cha Simba SC kimeanza safari ya kuelekea mjini Singida tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Big Stars utakaopigwa keshokutwa Jumatano (Novemba 09) mjini Singida.
Simba SC imesafiri kwa Ndege hadi Dodoma kisha itaelekea Singida kwa njia ya Barabara (Basi), kwa mchezo huo ambao umepangwa kupigwa katika Uwanja wa Liti, kuanzia saa kumi jioni.
Kikosi cha Simba SC kinaelekea Singida kikiwa na matumaini ya kuendeleza ushindi, kama kilivyofanya katika mchezo wake uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar, iliyokubali kichapo cha 5-0.
Hata hivyo Singida Big Stars inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, inajivunia ushindi ilioupata jana Jumapili (Novemba 05) dhidi ya Polisi Tanzania iliyokubali kulala 1-0, kwenye Uwanja wa Black Rhino mjini Karatu-Arusha.
Kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 17 sawa na Azam FC na Singida Big Stars, lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa inazitengatisha timu hizo katika nafasi ya pili na tatu.