Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kijana Jackson Majaliwa ambaye alifanikisha kuwaokoa abiria 24 wa ajali ya ndege iliyotokea Mjini Bukoba, kupewa ajira kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Majaliwa, ameyasema hayo hii leo Novemba 7, 2022 wakati wa ibada maalum ya kitaifa ya kutoa heshima za mwisho kwa miili 19 ya waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea jana Jumapili (Novemba 6, 2022).
Amesema, pamoja na mambo mengine, kijana huyo atapewa mafunzo zaidi ya uokoaji na kujengewa ujasiri wa kushiriki shughuli mbalimbali za uokoaji na kusema Serikali inatambua juhudi na jitihada za wavuvi wengine waliosaidia uokoaji.
“Rais Samia ameguswa na ujasiri wa kijana huyu na ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kumwajiri katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa ajili ya mafunzo zaidi na kumjengea ujasiri,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha Majaliwa ameongeza kuwa, “Nakuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani kutekeleza hilo haraka kwa kuchukua maelezo yote muhimu ya kijana huyu jasiri kwa hatua zingine.”
Awali, kijana huyo alikabidhiwa zawadi ya Shilingi milioni 1 kama ishara ya kutambua juhudi na moyo wake wa kujitolea zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila huku Serikali kisema itagharamia mazishi ya wote waliopoteza maisha katika ajali hiyo.