Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amesema Serikali imewashika mkono wa pole kwa kutoa Shilingi Milioni 1 kwa familia 19 zilizofiwa na wapendwa wao kutokana na ajali ya Ndege iliyotokea mjini Bukoba, ili kusaidia shughuli za msiba.
Pamoja na ubani huo, pia Serikali pia imesema italipia gharama zote za mazishi za watu hao wanaotarajiwa kuzikwa maeneo mbalimbali nchini kama ambavyo familia za marehemu zitakavyoelekeza.
Katika ibada maalum ya kuwaaga marehemu hao, iliyofanyika hii leo Novemba 7, 2022 ya kutoa heshima za mwisho kwa waliofariki, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa husika kusimamia utekelezaji wa agizo la kugharamia mazishi.
Shughuli ya kuaga na kutoa heshima za mwisho zimefanyika katika uwanja wa Kaitaba kabla ya miili ya marehemu kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa taratibu za kifamilia.
Ajali hiyo iliyokea baada ya ndege hiyo mali ya shirika la Precision Air kutua na kuzama ndani ya maji ya Ziwa Victoria, huku uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo ukiwa unaendelea.